MIAKA 19 HATUNAYE MWALIMU, LAKINI FIKRA ZAKE ZINAISHI

IMG_20181006_170502_4_1538976216913_1538992925523
Mwandishi wa Makala hii Jabiri O. Makame, akisoma moja ya vitabu vinavyomzungumzia Hayati Mwalimu J. K. Nyerere katika maktaba yake ya nyumbani.



Na Jabiri O. Makame

Ilikuwa siku ya Alhamisi majira ya saa 5 asubuhi, siku ambayo haijawahi kupotea kwenye fikra zangu, nikiwa mwanafunzi wa darasa la 4 katika Shule ya Msingi Luchelegwa, iliyopo wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi. Hali ikiwa shwari na kwa mbali zilisikika sauti za ndege waliokuwa wakiranda kwenye miti iliyopandwa kwa ustadi wa aina yake, hivyo kuifanya shule hiyo kuwa na mandhari ya kuvutia. Walimu na wanafunzi, kila mmoja kwa nafasi yake alikuwa katika hekaheka ya kutimiza wajibu wake kwa ujenzi wa taifa. Ghafla mlio wa kengele ulisikika kuashiria wito wa dharula kupokea taarifa kutoka kwa walimu. Bila shaka kwa wale waliowahi kupitia shule kama hizi watakubaliana nami kwamba hakuna wakati mzuri ambao unaleta faraja, kama pale unaposikia taluma likipigwa muda usio wa kawaida hivyo kukupa wazo kwamba mnaruhusiwa kurudi nyumbani hadi siku nyingine.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa wanafunzi wa shule hii kongwe. Shangwe, vifijo na nderemo vilisikika kutoka kila darasa na sote tulikusanyika pamoja huku tukisubiri kwa shauku kubwa kusikia kilichojiri kwa siku hiyo.
Furaha, vifijo na nderemo zetu zilizimwa ghafla na sauti ya simanzi ya aliyekuwa Mwalimu Mkuu wetu Ndugu Hassan Malunga ambaye kwa majonzi alitoa taarifa iliyotufanya tububujikwe na machozi. Hali hiyo ya huzuni ilitamalaki kwa wananchi wote wa kijiji kile na kila mahali watu walipokutana hapakuwa na mazungumzo yeyote isipokuwa mjadala wa kutoweka kwa nuru ya matumaini iliyoangaza Tanzania, Afrika na Duniani kote. Kwa hakika tukio hili lilionesha ni kwa namna gani mwalimu alikuwa mtu wa watu kiasi cha kuvuta hisia za watu wa rika zote hata vijana wadogo ambao kwa umri wetu tulikuwa bado hatujamfahamu kwa undani Mwalimu Nyerere. Mwalimu alikuwa zaidi ya kiongozi. Alikuwa baba, babu na mlezi wa karibu wa watanzania na Afrika.
TZ2-413x524
Kutoweka kwake kulijenga hofu miongoni mwa watanzania na kila mmoja aligeuka kuwa mtabiri wa maisha ya Tanzania bila mwalimu Nyerere. Kwa masikio yangu nilisikia minong’ono ya hapa na pale na kwa macho yangu niliona sura za wananchi zilivyokuwa na hofu. Wapo walidhani kuna vita inakuja mbeleni na wapo walidiriki kunena Tanzania bila Mwalimu haiwezi kufika. Kwa umri wangu kipindi hicho sikung’amua kwa nini watu walikuwa na mawazo hayo, baadae kidogo nilibaini kwamba hofu ile ilitokana na jitihada ambazo Mwalimu alizifanya katika kujenga umoja na mshikamano kwa kupiga vita mambo yote ambayo yanaweza kututenganisha kama vile udini, ukabila na ukanda. Kwa kushirikiana na Hayati Shekh Amani Abeid Karume, waliijenga Tanzania juu ya misingi iliyowekwa na TANU na ASP, ya kwamba binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja. Sura zao na vitendo vyao vilisadifu maneno yao, hivyo kuziteka fikra na mawazo ya wananchi wao. Hii ndiyo tasfiri halisi ya uongozi.

Siku, miezi na miaka imeyoyoma na hatimaye leo Oktoba 14, 2018 tumetimiza miaka 19 tangu Baba wa Taifa atutoke. Ingawa kimwili hatuko naye, taifa letu bado linajivunia tunu alizotuachia za umoja na amani ya Taifa letu. Ustawi wa tunu hizi na kusambaa kwa matawi yake umetokana na mbegu bora ambayo aliipanda, na kuipalilia kwa miaka kadhaa kabla ya kifo chake. Mti huu bora duniani unaendelea kustawi, kunawiri na matawi yake kushamiri kwa nchi jirani na Afrika kwa ujumla. Sote kama taifa hatuna budi kuienzi na kuidumisha kwa ustawi wa Tanzania ya sasa na baadae.
Aidha, tunapotimiza miaka 19, tangu baba wa Taifa atuache, pamoja na kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, hatuna budi kufanya tafakuri ya kina juu ya barugumu la pili lililopulizwa na Mwalimu mara baada ya uhuru kuwataka watanzania kulinda uhuru wetu. Mwalimu na waasisi wote wa bara la Afrika walifanya kazi ya kupigania uhuru wa kisiasa na kutuachia jukumu la kupigania uhuru wa kiuchumi kwani hatuwezi kulinda uhuru wetu wa kisiasa kama taifa letu haliwezi kujitegemea.

Katika Azimio la Arusha (1967) Mwalimu alisisitiza ya kwamba uhuru unamaana kujitegemea, uhuru hauwezi kuwa wa kweli kama taifa litakuwa linategemea zawadi na mikopo kutoka nchi nyingine kwa maendeleo yake. Hata kama kungekuwa na taifa au mataifa ambayo yako tayari kutupatia fedha zote tunazotaka kwa ajili ya maendeleo yetu, isingekuwa sahihi kwa sisi kukubali msaada huo bila kujiuliza wenyewe ya kuwa misaada hii inamadhara gani kwa uhuru wetu na namna tutakavyoishi kama taifa. Aidha katika Kitabu cha “Dead Aid” Dr. Dambisa Moyo anaeleza kuwa kamwe Afrika haiwezi kutoka katika dimbwi la umasikini kwa kutegemea misaada na mikopo kutoka kwa wahisani mpaka pale nchi za Afrika zitakapoamua kwa dhati kujiletea maendeleo wao wenyewe. Katika jitihada za kupambana na mfumo kandamizi wa kibepari Prof. Yash Tandon katika kitabu chake “Trade is War”, anaeleza kiunagaubaga namna ambavyo mataifa ya kimagharibi yanatumia udhaifu wetu kiuchumi (utegemezi) kutunyonya kupitia mashirika ya kimataifa na mikaba mbalimbali.
Hivyo, katika kuenzi fikra za baba wa Taifa kulinda Uhuru wetu, leo tunapofanya tafakuri ya miaka 19 ya kifo chake, watanzania hatuna budi kutembea kifua mbele kwa jitihada kubwa zilizofanyika chini ya viongozi wetu Rais Mstaafu Alhaji Ali Hassani Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na hasa, awamu ya tano chini ya Mh. Dr. John Pombe Magufuli, kwa kutembea katika misingi ambayo baba wa taifa aliisisitiza. Nia na maono ya serikali ya awamu ya tano ni kuifanya Tanzania kujitegemea kiuchumi. Kwa kauli na vitendo vya kiongozi wetu Dr. Magufuli na wasaidizi wake Mama Samia Suluhu na Kassim Majaliwa, wanaonesha nia ya dhati kuirudisha Tanzania katika misingi ambayo baba wa taifa aliisisitiza. Mapambano dhidi ya Rushwa, Mikataba mibovu ndani ya sekta ya madini na sekta nyingine, nidhamu ya matumizi ya fedha za umma sambamba na kupigania maslahi ya wanyonge walio wengi ni matendo ambayo yanalenga kujenga heshima ya Taifa letu.
vlcsnap-2015-12-09-11h30m32s157
Wapo wanaobeza jitihada hizi lakini hatupaswi kurudi nyuma. Mabadiliko yeyote katika jamii lazima yaambatane na maumivu ambayo yatazaa matokeo chanya kwa mustakabali wa Tanzania ya leo na baadae.
Nazifananisha jitihada za Rais Magufuli na jitihada zilizofanywa na Hayati Lee Kuan Yew, aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Singapore ambaye ameipaisha Singapore kutoka nchi masikini kuwa nchi tajiri. Alipochukua madaraka mwaka 1959 chini ya Chama Chake chenye itikadi ya mlengo wa kati kulia PAP (The People’s Action Party), aliikuta Singapore ikinuka rushwa, uzembe na umangimeza serikalini, hali mbaya ya uchumi, matumizi mabaya ya rasirimali za umma, mikataba mibovu na wananchi waliishi katika umasikini uliyokithiri. Kama ilivyokuwa kwa Rais Magufuli, wakati wa kampeni na siku aliyoapishwa, Lee Kuan Yew alijipambanua kwamba serikali yake ni serikali ya usafi kwa maana usafi wa utendaji wa shughuli zote za serikali, usafi wa wananchi na usafi wa mzingira. Alifanya maamuzi magumu ambayo yaliwaumiza wachache hata wale waliokuwa ndugu na rafiki zake wa karibu, lakini yalikuwa na manufaa kwa walio wengi. Na leo Singapore ni miongoni mwa nchi zilizo na uchumi imara duniani.

Hivyo, kumuezi baba wa Taifa kuna gharama zake za kuwa tayari kukubali kubadili baadhi ya mienendo yetu ambayo inarejesha nyumba maendeleo yetu. Kila mtanzania hana budi kuunga mkono jitihada za kizalendo zinazofanywa na serikali ili ifike wakati taifa letu lisimame imara kiuchumi kisiasa na kijamii. Leo na siku za usoni kila mwananchi na kila mtanzania katika kila jambo analotenda hana budi kujiuliza je, matendo hayo anayofanya yanakwenda sambamba na jitihada za serikali ya awamu ya Tano zenye lengo la kuijenga Tanzania mpya hasa kuinua maisha ya wananchi wanyonge? Kama jibu ni ndiyo basi matendo hayo hayana budi kuendelezwa na kama jibu ni hapana, basi matendo hayo yafaa kuepukwa. Kama asemavyo Mwalimu, kwamba “kitakachotuwezesha kujenga nchi safi siyo tamaa yangu mimi kuwa tajiri, bali ni vitendo ambayo japo vitawaudhi ndugu zetu wachache lakini vina manufaa kwa walio wengi”. Kadhalika asemavyo, Hayati Nelson Mandela ya kwamba “Taifa lolote halipimwi kwa namna linavyowajali na kuwatendea wananchi wa tabaka la juu bali kwa namna linavyowatendea wale walio chini”. Hizi ndiyo fikra za serikali yetu na mwelekeo tunaopaswa kuelekea kama Taifa. Ni ukweli usiopingika kwamba, kimwili hatuko naye Mwalimu, lakini kifikra na matendo tunamuona kwa Rais wetu, Dr. John Pombe Joseph Magufuli. Pumzika kwa amani baba yetu Mwalimu J. K. Nyerere. Nchi uliyoiasisi bado ipo katika mikono salama.
Mwandishi wa Makala hii ni Afisa Tawala, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala na Mchambuzi wa Masuala ya Siasa na Uongozi.
Anapatikana kwa: Namba +255 753 276347
Barua Pepe; jabirimakame@ymail.com

Comments

Popular posts from this blog

ARCHBISHOP TUTU FELLOWSHIP PROGRAMME FOR AFRICAN YOUNG LEADERS 2019

The Yale Young African Scholars Program 2019 for Secondary School Students, is now open! Apply today!

GREAT TRIP TO SHANGHAI