TANZANIA YA KESHO IPO MIKONONI MWA WATOTO WAKE. TUNAWAANDAJE?
Na Jabiri O. Makame
Tarehe 16 Juni, Tanzania inaungana na mataifa mengine Barani Afrika KUADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA. Siku hii huadhimishwa kila mwaka ikiwa ni kumbukumbu ya vifo vya watoto waliouawa huko sowetho, Afrika Kusini wakiwa katika maandamano ya kupinga utawala wa kibaguzi wa makaburu. Siku hii hutumika kwa kufanya tafakuri juu ya haki mbalimbali za mtoto katika masuala ya malezi, makuzi, ulinzi na usalama wa mtoto.
Maamuzi ya kuadhimisha siku hii yalifanyika Novemba, 20, 1989 ambapo mkataba wa Kimataifa wa haki za watoto (Convention on the Rights of the Child) uliridhiwa katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa na Tanzania iliridhia mkataba huu mwaka 1991.
Maamuzi hayo yalifanyika kwa kutambua kwamba, hatma ya taifa lolote lile duniani inategemea aina ya malezi na makuzi yatolewayo kwa watoto. Taifa linalojali na linalotambua thamani ya mtoto wa leo kwa mustakabali wa taifa la kesho, daima huandaa mazingira wezeshi ya malezi na makuzi ya mtoto ili kumuandaa kuwa raia bora kwa taifa lake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba makuzi bora ya watoto hujenga taifa bora kinyume chake ni kujenga kizazi kisichojitambua na kuwajibika katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika taifa. Tanzania kama nchi yeyote ile, ili iweze kufikia malengo yake hasa katika jitihada za kimaendeleo haiwezi kukwepa jukumu la kuwaandaa watoto katika nyanja zote zitakazowawezesha kuwa raia bora kwa mustakabali bora wa Taifa.
Kwa kutambua ukweli huo, Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kisera na sheria ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki kwa ustawi wa mtoto. Nia na dhamira hii ya serikali inajidhihirisha katika mamuzi ya kuridhia mikataba mbalimbali ya kulinda haki ya mtoto ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa haki za watoto (Convention on the Rights of the Child) ulioridhiwa katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa Novemba 20, 1989 na Tanzania kuridhia mwaka 1991.
Pamoja na mkataba huu, Tanzania imesaini mikataba mingine ya kuwalinda watoto ikiwemo Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto ( African Charter on the Rights and Welfare of the Child) wa mwaka 2003, Itifaki ya Hiari kuhusu Usafirishaji wa Watoto, Ukahaba wa Watoto na picha za Ngono wa mwaka 2003, Itifaki ya Hiari Kuhusu Kupiga Marufuku Kuwahusisha Watoto katika Vita ya mwaka 2004 na Mkataba wa Kuondoa Aina zote za Ubaguzi kwa Wanawake na Watoto (CEDAW).
Kwa upande mwingine Tanzania inaendesha jitihada za kulinda haki za watoto kupitia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2009, Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2010 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa Watoto Waishio Katika Mazingira Magumu.
Ili kupata matokeo chanya kazi hii haiwezi kuachwa kwa serikali pekee, zipo taasisi binafsi, kampuni na watu ambao wamekuwa wakijitoa kwa hali na mali ili kumtoa mtoto katika mazingira hatarishi kwake ambayo yanaweza kuharibu hatma yake na hatma ya nchi yake. Taasisi za usimamizi wa sera na sheria zikiwemo wizara mbalimbali, idara kama vile Jeshi la Polisi, Mahakama, ustawi wa jamii ngazi za mikoa na wilaya zimekuwa zikitekeleza majukumu yao ili kufikia lengo la serikali.
Haya yote yanafanyika kwa kutambua umuhimu wa kundi hili nyeti kwani kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, zaidi ya 50% ya watanzania ni watoto (chini ya umri wa miaka 18). Hivyo, mipango na mikakati hiyo ina umuhimu mkubwa katika kuamua hatma ya Tanzania ya miaka 100 ijayo.
Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo ambazo zimekuwa zikichukuliwa bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili watoto. Tafiti na ripoti mbalimbali kuhusu haki na usalama wa watoto zinonesha kwamba bado tuna safari ndefu kufikia kilele cha mafanikio ya ukombozi wa watoto kwani bado kuna vitendo vya unyanyasaji, ukatili na uonevu dhidi ya watoto katika jamii.
Watoto wengi hunyanyaswa kijinsia kabla ya kutimiza miaka 18. Zipo jamii ambazo zinaendeleza mila na desturi potofu za ukeketaji, kutotilia maanani elimu kwa mtoto wa kike na unyanyasaji wa watoto yatima. Ajira za watoto bado ni tatizo, na ukizunguka kwe miji na majiji utakutana na mamia ya watoto ambao wanajihusisha na shughuli za ombaomba barabarani hivyo kuhatarisha maisha yao na kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Zipo sababu nyingi zinazokwamisha jitihada hizi zikiwemo udhaifu wa sheria na usimamizi wake, uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa malezi kwa watoto na taratibu za sheria za kushughulikia ukiukwaji wa haki za watoto sambamba na msingi dhaifu katika ngazi ya familia unaotoa mwanya kwa mtoto kukosa haki zake. Kati ya sababu hizo, familia huchangia kwa kiasi kikubwa katika kumjenga au kumharibu mtoto. Familia ndiyo taasisi ya kwanza na muhimu katika kumkuza na kumuandaa mtoto kuwa raia mwema. Kwa maana nyingine msingi wa malezi ya mtoto ni ngazi ya familia. Hivyo, changamoto nyingi zinazowakumba watoto chanzo chake ni familia kushindwa kutimiza wajibu wa msingi. Pamoja na mambo mengine mifarakano ya ndoa na jukumu la malezi kuachwa kwa mzazi mmoja, wazazi kukwepa jukumu la malezi na kuwaacha watoto wao wakilelewa na bibi na babu zao ambao uwezo wao wa kusimama katika misingi bora umepungua, hulka za kujali starehe zingine kuliko kukaa karibu na watoto sambamba na uzembe wa baadhi ya wazazi kukimbia majukumu yao ya msingi ya malezi. Hatimaye, watoto hutumikishwa kingono katika umri mdogo na hatimaye mimba za utotoni na kuambukizwa maradhi, kukosa elimu, baadhi ya wakina mama kujiingiza katika tabia hatarishi za kuuza miili ili kukidhi mahitaji ya mtoto baada ya kutelekezwa na baba.
Katika mazingira ya namna hii, jamii haipaswi kuwa kimya, na katika kutafuta mwarobaini wake lazima kuanzia katika mzizi ambao ni ngazi ya familia kwani msingi imara au mbovu huanzia katika ngazi hii. Aidha, jamii kwa ujumla tuna kila sababu kila mmoja kubeba jukumu la ulezi popote alipo.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu aliwahi kusema “…sote ni wazazi, watoto ni zawadi ya Mungu. Sisi pia tulikuwa watoto na tulitunzwa. Tusingetunzwa tusingekuwa hapa leo. Katika nafasi au hadhi yoyote uliyonayo, tusingetunzwa usingekuwa hapo leo. Hatuna budi kutunza zawadi tunayopewa na Mungu”
Hivyo, tuna wajibu wa ziada kuhakikisha kwamba watoto wanatunzwa, wanalelewa katika mazingira rafiki na kuandaliwa kuwa Raia bora kwa Taifa lao. Jukumu hili haliwezi kufanikiwa kama hakutakuwa na jitihada za pamoja kati ya jamii na serikali. Serikali imefanya jitihada kubwa ya kutengeneza mazingira bora ya kisera na kisheria ya kumtunza na kumlinda mtoto. Tatizo tulilonalo ni katika utekelezaji na usimamizi wa Sera na sheria ili kuleta matokeo chanya. Ni wakati muafaka sasa kwa wasimamizi na watekelezaji wa Sera na sheria hizo kuongeza jitihada katika usimamizi wa Sera, sheria na kanuni zake pamoja na kuzifanyia marekebisho ili kuzipa meno zaidi. Taasisi za usimamizi wa masuala haya ziimarishwe na zijengewe uwezo zaidi wa kimafunzo, rasirimali watu na rasirimali fedha ili zimudu kutekeleza majukumu yao ipasavyo, hatimaye tulinusuru Taifa la kesho.
Aidha jamii ina wajibu wa ziada kutembea katika nyayo na msemo wa Mke wa Rais Mstaafu Mama Salma Kikwete ya kwamba “Mtoto wa mwenzio ni wako”. Kila mmoja kuanzia katika familia aone kwamba kumyanyasa na kumdhalilisha mtoto ni kuhatarisha uhai wa Taifa letu. Kila mmoja awe tayari kutoa taarifa za vitendo vyovyote vya ukatili, uzalilishaji na unyanyasaji dhidi ya mtoto. Tukifanya hivyo, vita ya kupambana na vitendo hatarishi dhidi ya mtoto itaibuka na ushindi.
Mtoto ni Taifa la leo, mtoto ni Taifa la kesho. Sote kwa pamoja tumtunze, tumlinde, tumthamini na tumuandae kuijenga Tanzania kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni. Tanzania ya viwanda inategemea maandalizi bora ya mtoto wa Leo.
Mwandishi wa Makala hii ni Afisa Tawala katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, na Mchambuzi wa masuala ya Kisiasa, Uongozi na Kijamii.
Anapatikana kwa namba: +255687672312/+255753 276347
Barua Pepe: jabirimakame@ymail.com
Comments
Post a Comment